WANAFUNZI WA VYUO VIKUU DODOMA WAMRUSHIA BOMU LOWASSA
Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu dodoma wapinga habari zilizoenea kwenye vyombo vya habari na katika mitandao ya kijamii kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu Dodoma wamtaka LOWASSA achukue form ya uraisi.
Akiongea na vyombo vya habari ndugu
DANIEL DANIEL
-Rais wa
Saint Jonh’s University
26/03/2015
alisema kuwa:
Ndugu Waandishi wa habari, Tunapenda kutanguliza shukrani za dhati
kwenu kwa kufika katika eneo hili kutusikiliza.Mbele yenu ni viongozi wa
serikali za wanafunzi kutoka Vyuo vikuu mbalimbali vilivyopo mkoani
Dodoma.Ndugu waandishi wa habari,si kawaida na wala mazoea kwa marais na
viongozi wa serikali za wanafunzi kutoka vyuo tofauti kukutana kwa pamoja na
kuzungumza na nyie wanahabari kama inavyotokea hii leo.
Ndugu wanahabari,siku ya Jumapili ya tarehe 22 mwezi huu wa 3,kundi
la watu waliojitambulisha kama ni wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma
walijikusanya nyumbani kwa mh; Lowasa na kutoa matamko mbalimbali ikiwa pamoja
na kuutangazia uma wa watanzania kuwa sisi wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma
tunamuunga mkono na tunahitaji Lowasa awe rais wetu sambamba kumchangia pesa.
Ndugu wanahabari,Tunapenda kukanusha kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu
vya Dodoma kwa ujumla wetu hatukuhusika na jambo lile na kama viongozi wa
serikali za wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya mkoa huu wa Dodoma,Tunapinga na
kulaani kitendo cha watu wachache kwenda kutuingiza sisi wanafunzi wa vyuo
vikuu vya Dodoma katika jambo ambalo halituhusu na wala si lililotuleta hapa
Dodoma.Sisi kama wasomi ambao jamii inatutegemea kama kioo hatuwezi kuandamana
na kujikusanya kwenye nyumba ya kiongozi na kumuomba agambee urais, wakati
tunajua fika sisi hatuhusiki na uteuzi wa wagombea ndani ya taasisi
yao.Kilichofanyika ni kuudanganya uma wa watanzania na taasiasi yake kupitia
kivuli cha vijana wachache kutoka vyuo vya hapa Dodoma,waliolipwa pesa ili
waweze kuwa kava la tukio lile.
Ndugu wanahabari,Mkoa wa Dodoma unavyuo vikuu visivyopungua 8,Na jumla
ya wanafunzi wote tunaosoma katika vyuo vya Dodoma ni zaidi ya wanafunzi 35,000.Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) pekee
yake kinawanafunzi wasiopungua 22,000.Idadi ya watu waliojikusanya nyumbani kwa
Mh: Lowasa siku ya tarehe 22-03-2015 haizidi watu 230 wakiwemo Wamachinga na
Wenyeviti wa Jumuiya za wazazi, kama vyombo vya habari vilivyoripoti. Ukiwatoa
Wamachinga na Wenyeviti wa Jumuiya za wazazi waliotoka mikoa mbalimbali,idadi
ya wanafunzi waliokuwepo kwenye tukio lile hawazidi 150.Idadi hii ni sawa na asilimia
0.4 ya wanafunzi wote wanaosoma vyuo vikuu vya Dodoma.Ndugu wanahabari,kwa
akili ya kawaida kabisa asilimia 0.4 ya wanafunzi wa vyuo vikuu ndio waliokuwa
pale.Tunashangazwa na dhambi tusiyoitenda tunayobebeshwa wanafunzi wa vyuo
vikuu vya Dodoma ambao kwa sasa tupo bize na msimu mpya ya masomo wenye
changamoto mbalimbali.
Ndugu wanahabari,sisi kama vijana wasomi na watu tunaotegemewa na
jamii zetu tutakusanyika katika kujadili na kuchambua changamoto mbalimbali
zinazoikabili jamii yetu na sio kukusanyika kwa ajili ya mwanasiasa ambaye sifa
zake na uhadilifu wake unatiliwa shaka katika jamii.Tunaomba mlijulishe Taifa,
kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma hatujahusika na tukio lile isipokuwa
wanafunzi wachache walitumika kwa kupewa pesa na wahusika wa tukio
lile.Tunataka Taifa lijue hatupo tayari kutumia elimu zetu kulitia upofu taifa
letu.Waambieni mama zetu na baba zetu huku vijijini kwetu kuwa tumekuja
kutafuta elimu ili ituwezeshe kuwakomboa wao na sio kutumika na Wanasiasa kwa
malengo yao.Tunatambua haki ya mwanafunzi kuamua na kufanya shughuli za kisiasa
nje ya maeneo ya vyuo, lakini hatukubaliani na wanafunzi wachache kuchafua na
kuwapaka matope maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma ambao hawajahusika
na tukio lile.Hii sio haki na haikubaliki.
Vilevile tungependa kutumia fursa hii kuwaasa wanafunzi wenzetu
popote pale nchini, makundi mbalimbali ya kijamii (wakulima, wafugaji, wavuvi,
wamachinga, wasanii, n.k), zikiwemo taasisi za dini kwamba watu wachache
kuzungumza kwa niaba ya makundi juu ya mambo yanayogusa maamuzi ya mtu binafsi.
Mwisho tunatoa wito kwa wanafunzi wenzetu wote kujitambua na kutumie
muda wetu kwa mambo ya msingi na muhimu kwa ustawi wa Nchi yetu. Na kuonesha
jinsi wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Dodoma walivyokasilishwa na jambo hili, Tamko
hili limesainiwa na wanafunzi 7821 toka vyuo mbali mbali vya Dodoma.Majina ya
sahihi za wanafunzi zimeambatanishwa. Tusikubali kutumika na wanasiasa wa aina
hii..
Asanteni
Mungu ibariki Tanzania,Mungu vibariki vyuo vikuu vya Dodoma.
Kwa niaba ya wawakilishi wa serikali za Wanafunzi Chuo cha
Mipango,Chuo cha Madini, Chuo cha Hombolo,Chuo kikuu cha Dodoma(UDOM) na CBE.
No comments